BUSTANI

Responsive Advertisement

KILIMO CHA MATIKITI MAJI | MUDA MFUPI NA KIPATO NI KIZURI


 

 

KILIMO CHA MATIKITI MAJI

UTANGULIZI

Matikiti maji hulimwa kama zao la biashara katika sehemu nyingi duniani zenye hali ya hewa ya joto la wastani. Zao hili lina wapatia watu shughuri za kufanya na hivyo kuwapatia kipato kuanzia kwenye nyanja za uzalishaji hadi kwenye matumizi. Matikiti maji ni mojawapo ya jamii aina ya matunda au mbogaboga inayotambaa. Mimea hii inapatikana katika kundi linalojumuisha mimea mingine (curcubitaceae family) kama matango, maboga na maskwash (squash). 
Zao la tikiti maji ni mojawapo ya zao ambalo lina faida kubwa sana ukilinganisha na mazao mengine kwa muda mfupi. Katika shamba la ukubwa wa ekari moja (1 acre) lililoandaliwa vizuri, kupandwa na kuhudumiwa vizuri mkulima ana uwezo wa kuvuna kiasi cha tani 15-36, ambacho kitamsaidia kupata fedha za kukidhi mahitaji yake mbalimbali na kuondokana na umasikini.


UCHAGUZI WA ENEO

Matikiti maji husitawi katika maeneo yenye joto la wasitani yaani haihimili hali ya joto kali sana, baridi kali, mvua nyingi wala udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu. 

Joto: Matikiti hukua vizuri katika maeneo yenye joto la wastani wa nyuzi kati ya 21 - 30 sentigradi. Iwapo mitikiti itapandwa katika maeneo yenye joto chini ya nyuzi 15 za sentigrade huchelewa kuota. 

Mvua: Matikiti maji yanahitaji kiasi cha mvua kati ya millimita 400 - 600 kwa msimu. Mvua nyingi husababisha uwepo wa magonjwa ya fungasi na bakteria ambayo huathili mavuno. 

Hali ya Udongo: Kilimo cha matikiti huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile vile haihitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa. Hali ya udongo katika kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile vile wa kuhimili kwenye udongo wenye pH 5.0 

Mikoa ya Tanzania: Kilimo cha matikiti maji kinakubali vizuri kwenye ukanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi wa tatu mpaka wa tisa. 


Uandaaji wa Shamba
Fyeka vichaka na ng’oa visiki vyote. Katua kwa kina cha sm 22.5 kwenye Sesa. Kabla ya kupandikiza udongo utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa. Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa. Weka mbolea ya samadi debe moja kwa kila mita 10 za eneo. Tengeneza matuta katika sehemu ambayo ina majimaji.

Upandaji 
Katika shamba la ukubwa wa hekta moja kiasi cha kilo 3 - 4 cha mbegu kinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila shimo. Usipande katika kitalu kwasababu miche ya mitikiti huwa ni dhaifu sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu hivyo kupelekea kufa kwa miche hiyo. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa mita 1 hadi 2 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 - 3 kutoka mstari hadi mstari. 


Zingatia kutokutumia mbegu za tikiti ulilonunua (kwa ajili ya kula) kwasababu linaweza kuwa ni chotara (Hybrid) ambayo hupelekea kushusha kiasi na ubora wa matikiti yatakayo zaliwa kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2).

Mbegu za Matikiti 
Mbegu maarufu ya tikiti ni Sukari F1, hata hivo madukani zinapatikana nyingi bora na tofauti tofauti kama vile:

Upunguzaji Wa Mimea 
Mimea ya mitikiti huanza kuota, baada ya kama wiki 2 hivi. Hivyo katika mbegu mbili au tatu ulizopanda kata moja na uache ile miche yenye afya zaidi ndio uendelee kukua. Ni vizuri ukaacha miche miwili katika kila shimo.

Angalizo: Usinga’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki. Vilevile unaweza kupandishia udongo kwenye mashina ili kusaidia kupunguza maji kutuama kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza rutuba. Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea matikiti waya wa kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito wa matunda. Wakati mimea inapo anza kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe (kuielekezea) kwenye waya na kuifungia. 


Umwagiliaji 
Shamba linatakiwa limwagiliwe mara kwa mara wakati mvua zinapokosekana au wakati wa mvua chache. Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni katika kipindi cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya kuvuna. Iwapo kutakuwa na ukosefu wa maji kutasababisha kutengenezwa kwa matunda ambayo si mazuri na yenye umbo baya, pia kupungua kwa ukubwa wa tunda.

Angalizo: usimwagilie matikiti wakati wa jioni sana au usiku kwasababu inaweza kusababisha magonjwa ya majani kutokana na unyevu kukaa muda mrefu. Vile vile usimwagilie juu ya maua wakati wa asubuhi au jioni kwasababu unaweza kuzuia wadudu kama nyuki ambao ni muhimu sana wakati wa uchavushaji. 


Mahitaji ya Mbolea ya Matikiti
Wakati wa kupanda tumia DAP weka gram 5 kwa kwa kila shimo (lenye mbegu moja, na weka gram 10 au 15 kama kuna mbegu 2 au 3), hakikisha mbolea na mbegu havigusani. Wiki mbili baada ya miche yako kuota weka mbolea ya kiwandani NPK (Yaramila winner) gram 5 tena kwa kila mche, hakikisha unaichimbia chini na isigusane na mmea. Weka mbolea yenye Calcium kama Yaramila nitrabo au CAN gram 10 kwa kila shina unapoona matunda yameanza ili kusaidia kupata matunda makubwa na mazuri.

Kwa ekali 1 ya matikiti utahitaji mfuko mmoja wa DAP, mmoja wa NPK na mmoja wa CAN ikiwa utabakiza miche miwili kwa kila shimo.

Hivi ukiwa shambani unawezaje kupima gram 5 au 10 za mbolea? Ni vigumu lakini kwa makadirio ya karibu ujazo wa kifuniko kimoja cha maji safi au soda take-away ni sawa na gram 5 hivyo ili upime gram 10 jaza vifuniko viwili vya maji safi. Soma hapa mahitaji ya mbolea katika mahindi

Matandazo (Mulches) 
Matandazo ina maana ya kutumia nyasi na mabaki ya mimea mingine kufunika aridhi. Baada ya miche kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu vile vile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.
 
kilimo-bora-cha-tikiti-maji
Matikiti maji shambani

WADUDU NA MAGONJWA YA MATIKITI

Wadudu wa matikiti wako wa aina mbalimbali na wanaoshambulia sehemu za majani na maua, na wengine hushambulia matunda, pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea. 

Magonjwa kama ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy mildew) na mengine yathibitiwe kabla hayajaleta madhara kwenye mimea. Ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi. Dawa aina ya Mancozeb inaweza kutumiwa kuthibiti magonjwa hayo hapo juu.


Vilevile matikiti hushambuliwa na wadudu ambao hukaa katika majani, maua na matunda. Dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda. Soma hapa magonjwa ya nyanya na dawa zake

UVUNAJI NA UHIFADHI WA MATIKITI

Matikiti maji ni miongoni mwa mazao yanayochukua muda mfupi sana kukomaa. Kwa kawaida tikiki maji huwa tayari kwa kuvuna baada ya siku 80 hadi 100 baada ya kupanda. Vuna wakati tunda limeiva kabisa. Vuna kwa wakati unaofaa. Epuka kulijeruhi tunda. Hifadhi katika eneo lenye ubaridi nyuzi 15 hadi 20 C. Hifadhi vizuri, unyevua-anga (humidity) uwe 80 hadi 85%. Uza mara tu baada ya kuvuna shambani.

MCHANGANUO WA KIPATO CHA MATIKITI KWA UFUPI

Vitu vya kuzingatia:
  • Hekta 1 = Square meter 10,000
  • Ekali 1 = Square meter 4000
  • Hekta 1 = Ekali 2.5
Tuchukulie mathalani una ekali moja
Ukipanda matikiti yako kwa nafasi ya 1m x 2m utakua na mashimo 2000 ya kupanda mbegu zako. Ikiwa kila shimo utapanda mbegu tatu na ukapunguzia mche mmoja na kuacha miwili ikue basi utakua na mimea 2 x 2000 = 4000.

kwa hiyo kwa ekali moja utakua na mimea 4000 ya matikiti. haya tufanye umeipunguzia matunda na hivyo kuufanya kila mmea uzae matunda mawili tu hivyo tunatarajia utavuna matunda 2 x 4000 = 8000.

Hivyo basi katika ekali moja ya matikiti uliyopanda kwa nafasi ya 1m x 2m ukakuza mimea 4000 utapata matunda 8000!

Tuchukulie mathalani umeamua kuuza matikiti yako shambani kwa bei ndogo kabisa ya Tsh. 1000 kwa tikiti moja, ukiuza matikiti yote 8000 utapata jumla ya Tsh. 1000 x 8000 = Tsh. 8,000,000 (Milioni nane)! 

Inawezekana kabisa kuwa huu mchanganuo ni wa nadharia tu lakini ndugu yangu tumechukulia makadirio ya chini sana. Unajua ni kwanini? 

Angalia hapa: 
  • Mmea mmoja unaweza kuzaa matunda mangapi? We unajua lakini licha ya hayo yote sisi tumechukulia matunda mawili tu kwa mmea mmoja. 
  • Pia bei ya tikiti inategemea ukubwa wake lakini sisi tumechukulia yote ni sawa na tunauza kwa bei moja tu. 
  • Halafu pia bei ya matikiti tumechukulia ni Tsh 1000 tu wakati inaweza kuwa hadi Tsh 2000 uki-target wakati mzuri kwa soko.

Bila shaka utakuwa umenielewa vizuri sana, sasa fursa nimeiweka mikononi mwako na nimekufumbua macho yako, kazi kwako ndugu yangu. Lakini pia waweza kupitia namna ya kuzalisha matango na mananasi kisasa. Usisahau kuacha comment yako hapa chini.



Post a Comment

20 Comments

  1. Shukran kwa somo zuri pamoja na kutufumbua macho!!

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hakika watanzania tunakua masikini kwa kukosa maarifa

      Delete
    2. Nimefurahi sana kupata details hizi, je upatikanaji wa mbegu bora ni rahisi na hakuna makanjanja wa naouza mbegu fake?

      Delete
  2. asante kwa maelezo mazur mungu akubalik

    ReplyDelete
  3. This is a very useful article. Thank you.

    ReplyDelete
  4. Asante kwa elimu hii uliyotujuza

    ReplyDelete
  5. Nimepata Elimu nzur kuliko nilivyofikiro au kufanya, ubarikiwe kwa kunipatia ujuzi.

    ReplyDelete
  6. Shukran Sana kwa elim hii kk

    ReplyDelete
  7. Ahsante kwa elimu nzuri lakini kuna tatizo moja kwenye soko la matunda kama unavyo jua kilimo cha matunda ni ngumu sana kulitunza tunda hivyo basi punde baada ya kuvuna linatakuwa kuuzwa kwenye soko apo ndugu zangu tuna omba msaada .... hata Hivyo nashukuru sana kwa elimu nzuri 🙏

    ReplyDelete
  8. Sante sana kwa elimu nzuri mimi Ni mjasiriamali mdogo na nilipenda Sana kuanza kilimo hichi pia nipo mbeya unanishaurije

    ReplyDelete
  9. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  10. Elimu nzuri sana Mungu akubariki... Mimi nataka kufanya kilimo cha tikitiki ukubwa wa eneo langu ni 2000 sqrm naomba ushauri

    ReplyDelete
  11. Binafsi nimeelimika sana. Shukrani sana kwa somo zuri

    ReplyDelete
  12. Shukran Sana... *Thanks Alot 🙏*

    ReplyDelete
  13. Ni furaha ilioje.. kilimo ambacho hakina gharama kubwa ila faida yake ni kubwa zaidi.. NIMEJIFUNZA.. ASANTE..

    ReplyDelete